Chini ya kichwa cha habari "Tume ya Katiba haikutenda haki" gazeti la Tanzania Daima limetoa tahariri ifuatayo. Inashangaza ni kwa nini Tume imeshindwa kuwezesha magazeti mengine yasiyo ya serikali na lile la Mwananchi kuchapisha rasimu ya pili. Inahojiwa pia ni kama rasimu hii imewafikia watu wenye ulemavu wa kuona?
RASIMU ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imechapishwa jana kwenye baadhi ya magazeti baada ya kuwa imepitia
vigezo vya kisheria kama alivyoahidi Rais Jakaya Kikwete wakati wa
kuipokea Desemba 30, mwaka jana.
Rais aliwaahidi wananchi kuwa baada ya rasimu hiyo kuchapwa kwenye
gazeti la serikali kama sheria inavyoelekeza, itasambazwa kwenye vyombo
vya habari ili wapate kuisoma na kuijadili kabla ya Bunge la Maalumu la
Katiba kuanza mwezi ujao.
Hata hivyo tunapenda kueleza masikitiko yetu kwamba tumeshutushwa na
ubaguzi wa wazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa vyombo binafsi vya
habari. Tunasema ni ubaguzi wa wazi na wenye nia mbaya ya kuwanyima wananchi
haki yao ya kikatiba ya kuisoma rasimu na kuijadili kutokana na
kusambazwa katika vyombo vichache. Rasimu hii imesambazwa kupitia magazeti matatu tu ya Habari Leo na
Zanzibar Leo ambayo ni ya serikali na Mwananchi, ambalo ni la binafsi
wakati yako magazeti zaidi ya 10 yanayotolewa kila siku na mengine
kadhaa ya wiki ambayo kila moja lina wasomaji wake.
Kwetu huu ni ubaguzi wa makusudi wa tume ambayo kimsingi tunaamini
imepewa fedha za kutosha kufanya shughuli zake ili wananchi wapate
taarifa za kile kinachoendelea kuhusu mchakato mzima wa katiba yao.
Kama tume iliweza kuvitumia vyombo vyote vya habari kutoa taarifa zake
na matangazo ya kuwahamasisha wananchi wapeleke maoni yao, inakuwaje
leo iwanyime haki hiyo ya kupata rasimu kupitia magazeti hayo?
Hivi kwa mwananchi asiyesoma magazeti ya Habari Leo, Zanzibar Leo au
Mwananchi ina maana hana haki ya kupata rasimu ili aweze kuisoma na
kuijadili kwa ajili ya kuainisha kasoro kabla ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba kuketi na kupitia rasimu hiyo?
Yawezekana Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba
ilighafirika katika jambo hili, hivyo basi tuna imani kuwa wanaweza
kulisahihisha kwa kusambaza rasimu hiyo kupitia magazeti yote ili kuwapa
wananchi haki kama alivyoahidi Rais Kikwete. Tunachelea kuamini kama kigezo cha tume kutochapisha rasimu hiyo
katika magazeti yote ni uhaba wa fedha, kwani tunatambua kwamba Bunge
liliidhinisha mabilioni ya kutosha kwa chombo hicho ili kukiwezesha
kufanya kazi zake kwa ufasaha.
Kodi zinazotumika kutengeneza katiba zimetokana na wananchi wote,
hivyo hakuna sababu yoyote ya kuwabagua katika kuwafikishia taarifa
kuhusu maoni na mapendekezo yao waliyoyatoa kwa tume. Rasimu inapaswa kufikishwa kila mahala, mijini na vijijini, yako
maeneo magazeti hayafiki, hivyo ni vema zikasambazwa nakala za kutosha
ili wananchi waisome na kujadiliana badala ya kutaka kuwazima kwa
kuwapangia vyombo vya habari vya kupata taarifa.
No comments:
Post a Comment