Wednesday 5 June 2019

Changamoto, Maboresho na Mbadala Viti Maalumu: Utekelezaji Wa Kifungu Namba 168(a) Cha Ilani ya CCM-2015-2020


BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI NA KATIBU MKUU CCM


Na Victoria Lihiru 

Waheshimiwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Ilani ya CCM kupitia kifungu namba 168(a) inasema ‘Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya 2015 – 2020, Chama kitaielekeza Serikali kuendelea kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha wanawake kushika nafasi sawa (50/50) za uongozi katika vyombo vya maamuzi katika ngazi zote.’ Kifungu hiki kinaweka wazi nia ya CCM kuchukua hatua muhimu kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki kikamilifu katika ngazi za kutoa maamuzi.  Bunge kama chombo kikubwa cha maamuzi kuna uwakilishi wa wanawake upatao asilimia 37, asilimia 30 ikiwa ni wanawake waliopatikana kwa utaratibu wa viti maalum na asilimia 7 wakitokea majimboni. Ikimaanisha kuwa kuna upungufu wa wanawake kwa asilimia 13 ndani ya bunge ili kufikia 50/50 inayozungumziwa na kifungu cha 168(a) katika Ilani ya CCM. Kati ya madiwani wapatao 4000 nchini Tanzania, wanawake madiwani waliochaguliwa kutoka kwenye kata ni takribani 240 sawasawa na asilimia 5 tu. Tasnifu yangu ya Shahada ya Uzamivu inaangazia kwa undani masuala ya sheria zinazowawezesha au kuwakwamisha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi. Baada ya kuonana na wanawake wanasiasa ikiwemo madiwani na wabunge wa kuchaguliwa na wale wa viti maalum, matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa utekelezaji wa viti maalumu japokuwa umetuletea baadhi ya mafanikio, haufuati malengo ya kuanzishwa kwake; -

Changamoto za Viti Maalumu

Mosi, ni kuhusu hadhi ya viti maalum, kuna kanuni na miongozo inayozuia madiwani viti maalumu kuwa wajumbe katika kamati za maadili katika kata zetu. Katika Halmshauri nyingine kuna mazoea ya kutowarusu madiwani viti maalumu kuwa wajumbe wa kamati za fedha. Hata kwenye zile Kamati ambao wanawake viti maalumu ni wajumbe mfano kamati za Ukimwi, Huduma za Jamii, na Mipango Miji, wanawake hawa hawaruhusiwi kuwa wenyeviti wa kamati hizo. Pia kuna sheria zinazowanyima fursa madiwani viti maalumu kuwa meya, naibu meya, wenyeviti wa halmashauri za majiji, miji na wilaya. Madiwani viti maalumu hawaruhusiwi hata kukaimu uenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata ikiwa diwani wa kuchaguliwa ana udhuru. Kuna baadhi ya kata ni bora kwa mwenyekiti wa Kijiji ama mtaa kukaimu uwenyekiti wa kamati ya maendeleo ya kata kuliko diwani viti maalumu. Katika hili tukumbuke kuwa wabunge viti maalum nao ni madiwani katika kata zao. Kwa upande wa Bunge, ile kanuni ya kutoruhusu wabunge viti maalumu kupata fedha za maendeleo, na kifungu cha Katiba kinachowanyima fursa wabunge viti maalumu kuteuliwa kuwa waziri mkuu vinawaweka wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini. Kimsingi, sheria, kanuni na mazoea yanayowanyima wanawake viti maalumu fursa uongozi katika halmashauri na bunge, zinatoa taswira kuwa kama taifa tumewaweka wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini, na tumesha weka hitimisho kuwa wanawake viti maalum hawana uwezo wa kuongoza ama kuwa sehemu ya maamuzi fulani. Hii ni kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa viti maalumu chini ya kifungu namba 4 cha Mkataba wa Kuondoa aina zote za Ubaguzi dhidi ya wanawake maarufu kwa Kiingereza the Convention on the Elimination of All Forms of Discrimination against Women (CEDAW) wa mwaka 1979, ambapo Tanzania ni mwanachama. Mkataba huu unatambua viti maalumu kama hatua za mpito ambazo hazitakiwi kukumbatia ama kuleta unyanyasaji na unyanyapaa kwa wanawake.

Pili, viti maalumu vimekuwa vikiwanufaisha wanawake wachache licha ya lengo lake la kuwajengea uwezo na uzoefu wanawake wengi ili waende kwenye siasa za majimbo. Tangu kuanzishwa kwa viti maalum takribani miaka 34 iliyopita, mpaka sasa Tanzania ina wanawake asilimia 7 tu kutoka majimboni. Hivyo, kwa miongo takribani mitatu na ushee, na kama vikifutwa leo, viti maalumu vitakuwa vimefikia lengo lake kwa asilimia 7 tu. Moja kati ya mizizi ya tatizo hili ni kutokuwepo kwa ukomo wa muda kwa mwanamke mmoja kuwa mwakilishi kupitia viti maalumu. Ukomo wa uwakilishi wa viti maalumu, kama ungekuwa vipindi viwili tu, ungewezesha wanawake wengi kwenda kushindana majimboni/katani, na kutoa fursa ya kada nyingine ya wanawake kupata uzoefu wa kisiasa. Mpangilio huu ungesaidia kupiga hatua za msingi na za haraka katika kufikia 50/50.

Kuna hoja kuwa wabunge ni wabunge na madiwani ni madiwani, hivyo kama mbunge wa jimbo/diwani wa kata hana ukomo pia mbunge/diwani wa viti maalum asiwe na ukomo ikiwa tu ataendelea kushinda kura za wale wanaowapigia kura. Tukumbuke kuwa wanawake viti maalumu japokuwa wana majukumu ya kibunge/kidiwani pia wanatumikia lengo la nyongeza. Wako katika viti hivyo ili kupata uzoefu utakaowawezesha kushiriki katika siasa za ushindani, kwa hiyo wanawake wengi zaidi inabidi wapate fursa ya kupata uzoefu huo. Kuwekwa kwa ukomo wa kuwa mbunge wa kiti maalum kutaendana na malengo ya kuanzishwa vitu maalum katika kifungu namba 4 cha CEDAW kinachotambua juhudi hizi kuwa ni hatua za mpito ili kurekebisha changamoto ambazo zimekuwa zikiwakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika vyombo mbalimbali vya maamuzi. Kutokuwa na ukomo wa kisheria ama kikanuni kunawapa wanawake walio katika viti maalumu faida ya ziada katika kuendelea kuhodhi viti hivyo, kwa kuwa wana mtandao mkubwa katika chama na katika mabaraza ya wanawake ya vyama, faida ambayo wanawake wanaowania viti maalumu kwa mara ya kwanza hawana. Hili suala la uhodhi wa viti maalumu ni la vyama vyote, lakini kwa kutumia nafasi yake kama chama tawala CCM inawajibu wa kutenda kwa mfano, ili kuhakikisha viti maalumu vinatekelezwa kwa namna inayokidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake hususani kuwapa wanawake wengi fursa ya kupata uzoefu wa kisiasa kuelekea majimboni.

Maboresho Viti Maalumu

Kutokana na changamoto tajwa hapo juu, njia ya kwanza ya CCM kutekeleza ahadi yake katika kifungu cha 168(a) cha Ilani ya Mwaka 2015-2020 ni kuielekeza serikali hususani Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Ttawala Bora na Haki za Binadamu ili vijadiliane na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo kikatiba inamamlaka ya kupokea orodha ya wanawake wanaopendekezwa na vyama vya siasa kushika nafasi za viti maalumu kulingana na uwiano wa kura wanazo pata, kuwa ili kuendana na malengo ya uanzishwaji wa viti maalum, majina yanayopendekezwa kwenye Tume ya Uchaguzi yasiwe ya wale wanawake waliokwisha kuwa kwenye viti maalumu kwa Zaidi ya vipindi miwili.  CCM kama chama tawala kiwe mfano wa kuwapa kipaumbele na kuweka ulazima wa wanawake waliokaa viti maalumu kwa zaidi ya vipindi viwili ili wagombee majimboni. Nafahamu kuwa mabadiliko haya yatapata pingamizi kubwa, hasa kutoka kwa wanawake wenyewe, lakini ukweli utabaki kuwa ukweli. Hivyo basi, kama njia ya kuwapa motisha wanawake waliokaa kwenye viti maalumu zaidi ya vipindi viwili, kuwekwe hatua ya mpito, kwa wanawake hawa kuhakikishiwa kuwa ikitokea wameshindwa uchaguzi, basi watapewa kipaumbele katika nafasi za viti maalum zitakazopatikana kwa CCM. CCM ina fursa ya kuweka ukomo wa viti maalumu katika kanuni za uchaguzi ambazo naamini zitafanyiwa marekebisho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.

Napendekeza pia CCM ielekeze vyombo husika kufanya utafiti na majadiliano na vyama vya siasa ili kuweka Kanuni zitakazo tumika na vyama vyote katika kuwapata wanawake viti maalumu kwa kuwa kwa sasa kila chama kina utaratibu wake, suala linaloibua maswali juu ya upatikanaji wao. Japo inafahamika kuwa sifa ya mbunge ni kujua kusoma na kuandika, kwa upande wa viti maalumu hatua kwa hatua ya namna wanawake hawa wanavyopatikana ni muhimu katika kuwapa imani wananchi juu ya matumizi ya kodi zao kwa ongezeko la idadi ya wabunge wa viti maalumu. Pia kuhakikisha wanawake wanaochaguliwa wana sifa na uwezo wa kusaidia kufikia malengo ya kuanzishwa kwa viti hivyo.

Japokuwa maboresho hapo juu, yatavifanya viti maalum kuwa na tija na hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake. Kusipokuwa na juhudi za ziada, itachukua muda sana kufikia 50/50. Kama baada ya miaka 34 ya kuanzishwa kwa viti maalumu ni wanawake asilimia 7 tu ndio wameweza kushinda majimbo ya ubunge, hesabu ya haraka inaonyesha unahitaji miaka mingine 102 ili kuweza kufika idadi ya asilimia 50 ya wanawake bungeni, na hii ni katika mpangilio wa asilimia 30 viti maalumu na asilimia 20 kutoka majimboni. Hivyo kama CCM haitachukua hatua za ziada utekelezaji wa kifungu 168(a) kuhusu 50/50 ifikapo 2020 ni ndoto. Hivyo, sambamba na uboreshaji wa viti maalum, njia nyingine ya kuongeza idadi ya wanawake ni kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambapo kwa kutumia sheria mpya ya vyama vya siasa, ambayo inaweka sharti la vyama vya siasa kuanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine, usawa wa kijinsia, CCM inaweza kuishauri serikali imshauri Msajili wa Vyama vya siasa kuweka katika kanuni za sheria ya Vyama vya Siasa zinazo endelea kutungwa, kifungu kinacho hakikisha kuwa asilimia fulani ya wagombea ni wanawake, sana sana asilimia ishirini, ili kujazia nafasi inayo achwa na viti maalum. Itakuwa jambo la msingi, NEC wangetenga majimbo asilimia ishirini ambayo watagombea wanawake pekee. Hivyo kutakuwa na asilimia 30 ya viti maalum, asilimia 20 ya majimbo ambayo watagombea wanawake hivyo kutimiza 50/50. Mfumo wa kutumia viti maalumu sambamba na majimbo ya wanawake pekee inatumika katika nchi jirani kama Rwanda na Kenya.

Mbadala wa Viti Maalum

Japo viti maalumu vinaweza kuboreshwa kama ilivyopendekezwa hapo juu na kutuletea 50/50, kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kama bado tuna hitaji viti maalumu, au kama nchi tunaweza kuwa na mfumo bora wa kuwezesha wanaume na wanawake kushiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi. Nakumbuka imeshasemwa kuwa suala la katiba mpya, japo muhimu, lakini siyo kipaumbele kwa wakati huu. Hivyo mapendekezo hapa chini yanajikita kwenye uelewa kuwa yanaweza kuwekwa katika Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama mabadiliko madogo (miscellenious amendment) ili kuweka utaratibu utakaosaidia kuifikia 50/50. Nikiongozwa na usemi wa ‘Msema kweli ni mpenzi wa Mungu.’ Napendekeza kuwa viti maalumu vinahitaji mbadala haraka iwezekanavyo. Asimia 30 ya wanawake bungeni sio lazima iwe viti maalumu, inaweza ikatafsiriwa katika majimbo na kata, yaani asimilia 30 ya majimbo na kata zote za uchaguzi wagombea wawe ni wanawake peke yao, kila chama kisimamishe mwanamke kama mgombea katika majimbo na kata hizo. Na wale wanawake wenye uwezo wa kugombea katika majimbo yasiyo ya wanawake waruhusiwe kufanya hivyo. Japo pendekezo tajwa hapo juu ni zuri, lakini halitatufikisha kwenye 50/50 inayo ahidiwa na kifungu cha 168(a) cha Ilani ya CCM 2015-2010. Hii inanilazimu nitoe hoja mbili kama mbadala wa viti maalumu; -

Mosi, ni kugawanya idadi ya majimbo na kata zilizopo mara mbili (ili kutoongeza ukubwa wa bunge/baraza la madiwani). Katika kila jimbo na kata kila chama kinasimamisha mgombea mwanamke na mwanaume. Mpiga kura anapokuwa amechagua chama fulani anakuwa amechagua mgombea mwanamke na mwanaume kutoka chama hicho. Hivyo baada ya uchaguzi unapata uwakilishi wa 50/50 kwa wanawake na wanaume katika kata na majimbo. Mbadala wa pili, ni kubadili mfumo mzima wa uchaguzi kutoka utaratibu wa jimbo au kata moja kuwa na mwakilishi mmoja yaani First Past the Post (FPTP) mpaka uwakilishi wenye uwiano sawa yaani Proportional Representation (PR). Mfumo huu unatakiwa uende sambamba na sharti la kutaka orodha ya wawakilishi wa vyama katika majimbo na kata kuwa na idadi sawa ya wanawake kwa wanaume kwa kufuata mfumo wa pundamilia yaani Zebra System. Faida zinazoendana na kuweka mbadala wa viti maalumu, ni pamoja ya kuiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi. Hii ni kwa sababu wanawake watakuwa wakitokea katika asilimia kadhaa ya majimbo na kata halisi, na si kama nyongeza juu ya namba halisi ya madiwani au wabunge. Serikali itaokoa Trilioni za shilingi ambazo zinazitumia sasa katika kulipa mishahara, posho na vi-inua mgongo kwa wanawake viti maalumu wakiwa kama nyongeza ya wabunge na madiwani halisi. Pia mbadala huu utaondoa maswali kutoka kwa wana jamii ya je wanawake viti maalumu wanamwakilisha nani, kwa kuwa sasa watakuwa wanatokea kwenye majimbo na kata. Watapata haki ya moja kwa moja ya kupata fedha za maendeleo ya jimbo na wataweza hata kuwa waziri mkuu kwa kuwa wana vigezo. Changamoto za madiwani viti maalumu kutoruhusiwa kuwa wenyeviti/mameya wa halmashauri na kamati za kata, na masharti ya kutokuwa wajumbe katika kamati za maadili, fedha, na kukaimu uwenyekiti wa kamati za maendeleo ya kata zitaondoka.

Hitimisho

Katika harakati zangu na kuonana na kuchota maarifa na maono ya watu mbalimbali juu ya suala hili, kuna mtu alinambia kuwa ‘Chama kina vipaumbele vingi, kama suala halina madhara kwa chama, nguvu na msukumo wa kufanyia kazi suala hio inakuwa haipo.’ Najitolea kupuuza ushauri wake kwa kuwa naamini suala hili nyeti na lenye tija kwa wanawake, ambao ni walezi wa taifa hili, wapiga kura wengi na waaminifu. Nina Imani CCM chini ya uongozi wa Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake itafanyia kazi mapendekezo haya. Muda umefika tufunge huu mjadala ili wote wanawake na wanaume tubaki kuchapa kazi.


Wasalaam- Victoria Lihiru- Mwanafunzi shahada ya Uzamivu Chuo Kikuu Cape Town, Afrika Kusini.  Napatikana kupitia victorialihiru@gmail.com, +255 713 085 139

Saturday 19 January 2019

New Book: Peacebuilding in Contemporary Africa In Search of Alternative Strategies

I am so excited that the edited volume by my Professor Kenneth Omeje, in which I contributed a Chapter on South Sudan has been published by Routledge. I sincerely thank Prof. Omeje who has always trusted me since we first met in 2008. I was his undergraduate student in his Research Methods class. He has since then been my mentor both at the academic and spiritual level. 

My Chapter examines the relapse of South Sudan into armed conflicts and the interest-driven regional rivalries in the country. It contributes to the wider debate of peacebuilding and state building literature in Africa. 

You can order a copy of the book in the link provided. 

The book in general provides a much-need perspective from African scholars and will be of interest to students, researchers, policy makers and practitioners with an interest in promoting legitimate policy interventions and sustainable peace in Africa. 



[ZELEZA] Malawi’s Political Earthquake: Nullification of the Presidential Elections

By Prof Paul Tiyambe Zeleza  3/2/2020 The Malawian Constitutional Court has annulled last year's presidential election results....

Most Viewed