Kufuatia mgogoro mzito ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), nimetuma maoni yafutayo kwenye gazeti la Mwananchi. Chini ya kichwa cha habari Chadema yamtimua Dk. Kitila, Mwigamba.
Demokrasia ndani ya vyama vya siasa ni suala ngeni na gumu hususan
katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa nchi kama yetu ambayo tumekulia na
kulelewa katika mfumo wa chama kimoja na kutawaliwa na chama kimoja kwa
muda mzima wa uhuru wetu, utamaduni wa siasa ya vyama vingi bado
hujakita mzizi licha ya mabadiliko katika katiba mwanzoni mwa miaka ya
90. Minghairi ya hayo, yanayotokea Chadema ni moja wapo ya michakato ya
upevu na upanuzi wa mjadala wa demokrasia nchini. Kunao wanakubalina na
kunao wanapinga yanayotokea Chadema. Tuyachukulie yanayojiri ndani ya
Chadema kama hatua moja wapo katika demokrasia. Demokrasia, msingi wake
ukiwa katika vyama na asasi mbali mbali inajengwa kwa muda mrefu na sio
rahisi. Hatua tuliyofika ya vyombo vya habari na umma kujadili kwa hisia
kubwa yanayojiri ndani ya Chadema ni hatua nzuri. Tusiyachukulie tu
hivi hivi bali tuombe pia vyama vingine vipate kujadili wanachama wao,
kujadili mada za kitaifa na mustakabali wa nchi yetu kwa ari kama hii.
Upanuzi wa mijadala ndio msingi wa demokrasia. Mungu ibariki Tanzania.