Vyanzo: Nipashe na Chadema Blog
Katibu Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa,
amesema anaendelea kutishiwa kuuawa na vyombo vya usalama na kwamba
njama zote zinazopangwa dhidi yake amezibaini.
Hata hivyo, Dk.
Slaa amesema hataacha siasa kutokana na vitisho hivyo na yupo tayari
kufa kwa ajili ya kutetea umma wa Watanzania katika kupata haki yao
ikiwamo kunufaika na rasilimali zao ambazo zinanufaisha watu wachache.
Aliyasema
hayo katika viwanja vya Railway, Manispaa ya Moshi jana na katika
viwanja vya Kwasa Kwasa mjini Same wakati wa mikutano yake ya hadhara.
“Nimetishiwa
kuuawa zaidi ya mara tatu na hadi sasa wahusika wanaendelea na mipango
ambayo yote inavuja na kutufikia Chadema,” alisema na kuongeza:
“Sitaacha siasa kwa vitisho vyao ndiyo kwanza nasonga mbele nimejitoa
maisha yangu.”
Aliongeza kuwa bahati mbaya mipango inayopangwa
imekuwa ikivuja kwa kuwa nyumba yao inavuja na hivyo wenye uchungu na
nchi wamekuwa wakitoa taarifa hizo.
Alililaumu Jeshi la Polisi
kwamba linaminya demokrasia kwa kutolea mfano kitendo cha Jeshi hilo
kuwazuia vijana kutundika bendera za Chadema katika pikipiki juzi katika
Manispaa ya Moshi na jana mjini Same.
KAULI YA POLISI
NIPASHE
ilipomtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso,
kuzungumzia madai ya kiongozi huyo, alisema hajapata taarifa na kutaka
apelekewe ushahidi ofisini kwake.
“Mimi na wewe tuko Dar es Salaam, sasa tunayajuaje mambo yanayoendelea huko Kilimanjaro?” Senso alihoji na kuongeza:
Kama
wewe una ushahidi kuhusiana na taarifa hizo, ninaomba uniletee document
(nyaraka) kesho (leo) asubuhi ofisini kwangu zikiwa zinaonyesha
alizungumza wapi na tarehe ngapi.”
Licha ya NIPASHE kumsisitizia
kwamba Dk. Slaa alitoa kauli hizo katika mikutano ya hadhara ambayo
wengi walisikia, lakini hakukubali na kusisitiza kwamba apelekewe
nyaraka hizo ofisini kwake.
“Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya
usalama wa raia na mali zao na ofisi zao zipo wazi saa 24 nchi nzima,
hivyo kila mtu anaruhusiwa kutoa taarifa,” alisema.
Aliongeza: “Kwa kuwa wewe unataka kutoa taarifa, ninamuomba aje ofisini kwangu asubuhi,” alisisitiza.
Dk.
Slaa alipoulizwa na NIPASHE jana mjini Same kama amewahi kuripoti
matukio ya vitisho dhidi yake kwa vyombo vya dola, alisema hatakwenda
katika chombo chochote cha dola kwa kuwa hao hao ndiyo wanaotaka
kumdhuru.
KADI YA CCM
Alisema wanaoeneza
propaganda za kuwa ana kadi mbili ikiwamo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ni wapuuzi na wamekosa cha kuzungumza.
Alifafanua kuwa ni hiari ya anayejiunga na chama kingine kuamua kadi ya chama cha awali aliyonayo aifanye nini.
Kuhusu
mauaji ya watu katika mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Tabora,
Kamati Kuu ya Chadema imetoa muda (hakusema siku ngapi) kwa serikali
kuhakikisha inachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuunda tume ya kimahakama
ya uchunguzi wa mauaji hayo.
“Tumeipa serikali muda wa kuunda
tume hiyo na kuchukua hatua stahiki, vinginevyo nchi haitakalika,
viongozi wanahubiri amani ya kinafiki huku watu wakiuawa kama kuku, hadi
leo wameendelea kumkumbatia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, ambaye alikuwa umbali wa mita kumi wakati mwandishi
wa habari wa kituo cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi, anauawa,” alisema.
Alisema
kutokana na kelele za viongozi wa Chadema, dunia nzima imejua juu ya
mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja
wa Ulaya (EU), Marekani na Japan, wamejua na wanafuatilia kwa karibu.
Alisema
uwezekano wa baadhi ya viongozi kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa
ya Uhalifu (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi ni mkubwa na hawataacha
kupiga kelele kwa kuwa raia wanauawa hovyo.
“Tumeitaka serikali
kuwachukulia hatua mafisadi wote, vinginevyo hatutakuwa na muda wa
kuhurumiana wala kubembelezana, Katiba imetamka wazi kuwa jukumu la
kusimamia rasilimali za taifa ni la wananchi na si serikali, hivyo
tutasimamia na wanaosema wamechoka kusikia suala la mafisadi, wakae
chonjo kwani mpambano ndiyo kwanza umeanza,” alisema.
Dk. Slaa
alisema kuanzia Januari 26 hadi 28, mwaka huu, Kamati Kuu, Baraza Kuu la
Chadema, wataanza kutoa matamko makali dhidi ya serikali ya CCM kulaani
mambo ya ufisadi, mauaji ya raia na mengine ambayo yanairudisha nchi
kwenye umaskini wa kutisha.
UFISADI NA MAFISADI
Alisema
suala la kukwapuliwa kwa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya
Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sh. bilioni 133 na
mabilioni ya Tangold, ambazo zilichukuliwa na CCM kwa ajili ya kampeni
za mwaka 2005, hawataacha kulizungumzia kwani ushahidi wa fedha hizo
kukwapuliwa na wachache kwa manufaa yao upo wazi kabisa.
“Tunaitaka
serikali kuutumia Usalama wa Taifa na Polisi kulinda rasilimali zetu
zisitoreshwe nje ya nchi kama inavyofanyika kwenye sekta ya madini na
wanyama, badala ya kupoteza muda mwingi kuwafuatilia Chadema,” alisema.
Alidai shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa hivi karibuni nchini China,
ikiwa ni mali ya kiongozi mmoja wa ngazi za juu kwenye CCM, ambaye
hakumtaja kwa jina, ni ushahidi tosha kuwa ndani ya chama hicho hakuna
aliye msafi, bali wanaendelea kutafuna nchi huku Watanzania wengi
wakiteseka kwa umaskini wa kupindukia.
Alisema watatumia nguvu ya
umma kuhakikisha fedha zilizoporwa zinarejeshwa na ndipo watatoa elimu
bure kwa kila mtoto wa Kitanzania na kulipa mishahara ya walimu na
watumishi wengine.
Alitumia mkutano huo kujibu hotuba ya Meya wa
Manispaa ya Moshi, Michael Jaffary, aliyemtaka kuzungumzia suala la Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, Mkuu wa Wilaya, Dk. Ibrahim
Msengi, kuingilia kazi za Baraza la Madiwani na Mkurugenzi wa Manispaa,
Benadetha Kinabo, kukataa kutekeleza maagizo ya baraza.
Alisema
Sheria namba 19 ya mwaka 1999 inaeleza RC na DC ni wahamasishaji kwenye
halmashauri na vyombo vyenye maamuzi ya kisheria ni Bunge kwa ibara ya
63 na halmashauri za wilaya kwa ibara ya 45 na 46 na ndiyo maana vikao
vya viongozi hao ni vya mashauriano na haviwezi kuwa juu ya vikao vya
kisheria.
“Baraza la Madiwani ni Bunge kwenye eneo husika na
watatunga sheria zao, mna haki ya kusimamia haki za wananchi bila
kuyumbishwa, kama wanaendelea kuwasumbua, niiteni nije tuwashikishe
adabu kama nilivyofanya kwenye Halmashauri ya Karatu,” alitamba Dk.
Slaa.
Alisema suala la Mkurugenzi kukataa kusaini kutolewa kwa
Sh. milioni 216 kwa ajili ya kulipia ada ya watoto wa watu wasiojiweza
wapate elimu, ni maamuzi ya madiwani na kama Mkurugenzi huyo analipinga,
wamfungie nje bila kumuonea haya.
Awali, Mbunge wa Arusha Mjini
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema, Godbless Lema, alisema dhambi
ya woga inaitafuna Manispaa hiyo na Tanzania kwa ujumla kwani kama
Mkurugenzi anawasumbua wanaweza kumchukulia hatua kwa kuwa ni Katibu
kwenye vikao vya madiwani na anafanya kile anachoelekezwa na Baraza
linaloongozwa na Meya na theluthi ya madiwani wanatoka Chadema.
Meya
Jaffary katika taarifa yake, alisema Manispaa imefanikiwa kuongeza
mapato ya halmashauri hiyo kutoka Sh. bilioni 1.8 mwaka 2009/10 hadi Sh.
bilioni 4.1 mwaka 2012/13 kwa kuziba mianya ya wizi iliyofanywa huko
nyuma na fedha imeelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Meya huyo
alimuomba Dk. Slaa, kuhakikisha suala la mamlaka za chini za serikali
zinafanya kazi kwa mujibu wa Katiba na si kwa matakwa ya chama tawala
kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa manispaa hiyo anakataa kutoa fedha hizo
kwa madai kuwa siyo sera ya CCM.
Hivi karibuni, uliibuka mvutano
baina ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na madiwani wa Chadema kwa madai
kuwa wanaingilia utendaji wa Manispaa hiyo.
Pia madiwani hao wamekuwa wakivutana na Mkurugenzi wa Manispaa kwa madai kuwa anakaidi kutekeleza maagizo ya Baraza la Madiwani.