BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI NA KATIBU MKUU CCM
Na Victoria Lihiru
Waheshimiwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ilani
ya CCM kupitia kifungu namba 168(a) inasema
‘Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani ya 2015 – 2020, Chama kitaielekeza
Serikali kuendelea kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaowawezesha
wanawake kushika nafasi sawa (50/50) za uongozi katika vyombo vya maamuzi
katika ngazi zote.’ Kifungu hiki kinaweka wazi nia ya CCM kuchukua hatua muhimu
kuhakikisha wanawake na wanaume wanashiriki kikamilifu katika ngazi za kutoa
maamuzi. Bunge kama chombo kikubwa cha
maamuzi kuna uwakilishi wa wanawake upatao asilimia 37, asilimia 30 ikiwa ni
wanawake waliopatikana kwa utaratibu wa viti maalum na asilimia 7 wakitokea
majimboni. Ikimaanisha kuwa kuna upungufu wa wanawake kwa asilimia 13 ndani ya
bunge ili kufikia 50/50 inayozungumziwa na kifungu cha 168(a) katika Ilani ya
CCM. Kati ya madiwani wapatao 4000 nchini Tanzania, wanawake madiwani
waliochaguliwa kutoka kwenye kata ni takribani 240 sawasawa na asilimia 5 tu. Tasnifu
yangu ya Shahada ya Uzamivu inaangazia kwa undani masuala ya sheria
zinazowawezesha au kuwakwamisha wanawake kushiriki katika ngazi za maamuzi. Baada
ya kuonana na wanawake wanasiasa ikiwemo madiwani na wabunge wa kuchaguliwa na
wale wa viti maalum, matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa utekelezaji wa
viti maalumu japokuwa umetuletea baadhi ya mafanikio, haufuati malengo ya kuanzishwa
kwake; -
Changamoto za Viti Maalumu
Mosi,
ni kuhusu hadhi ya viti maalum, kuna kanuni na miongozo inayozuia madiwani viti
maalumu kuwa wajumbe katika kamati za maadili katika kata zetu. Katika
Halmshauri nyingine kuna mazoea ya kutowarusu madiwani viti maalumu kuwa
wajumbe wa kamati za fedha. Hata kwenye zile Kamati ambao wanawake viti maalumu
ni wajumbe mfano kamati za Ukimwi, Huduma za Jamii, na Mipango Miji, wanawake
hawa hawaruhusiwi kuwa wenyeviti wa kamati hizo. Pia kuna sheria zinazowanyima
fursa madiwani viti maalumu kuwa meya, naibu meya, wenyeviti wa halmashauri za majiji,
miji na wilaya. Madiwani viti maalumu hawaruhusiwi hata kukaimu uenyekiti wa
kamati ya maendeleo ya kata ikiwa diwani wa kuchaguliwa ana udhuru. Kuna baadhi
ya kata ni bora kwa mwenyekiti wa Kijiji ama mtaa kukaimu uwenyekiti wa kamati
ya maendeleo ya kata kuliko diwani viti maalumu. Katika hili tukumbuke kuwa
wabunge viti maalum nao ni madiwani katika kata zao. Kwa upande wa Bunge, ile kanuni
ya kutoruhusu wabunge viti maalumu kupata fedha za maendeleo, na kifungu cha
Katiba kinachowanyima fursa wabunge viti maalumu kuteuliwa kuwa waziri mkuu vinawaweka
wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini. Kimsingi, sheria, kanuni na mazoea
yanayowanyima wanawake viti maalumu fursa uongozi katika halmashauri na bunge, zinatoa
taswira kuwa kama taifa tumewaweka wanawake viti maalumu katika hadhi ya chini,
na tumesha weka hitimisho kuwa wanawake viti maalum hawana uwezo wa kuongoza
ama kuwa sehemu ya maamuzi fulani. Hii ni kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa
viti maalumu chini ya kifungu namba 4 cha Mkataba wa Kuondoa aina zote za
Ubaguzi dhidi ya wanawake maarufu kwa Kiingereza the Convention on the Elimination of All Forms
of Discrimination against Women (CEDAW) wa mwaka 1979, ambapo Tanzania ni mwanachama.
Mkataba huu unatambua viti maalumu kama hatua
za mpito ambazo hazitakiwi kukumbatia ama kuleta unyanyasaji
na unyanyapaa kwa wanawake.
Pili, viti maalumu vimekuwa vikiwanufaisha wanawake wachache licha
ya lengo lake la kuwajengea uwezo na uzoefu wanawake wengi ili waende kwenye
siasa za majimbo. Tangu kuanzishwa kwa viti maalum takribani miaka 34
iliyopita, mpaka sasa Tanzania ina wanawake asilimia 7 tu kutoka majimboni. Hivyo,
kwa miongo takribani mitatu na ushee, na kama vikifutwa leo, viti maalumu vitakuwa
vimefikia lengo lake kwa asilimia 7 tu. Moja kati ya mizizi ya tatizo hili ni
kutokuwepo kwa ukomo wa muda kwa mwanamke mmoja kuwa mwakilishi kupitia viti
maalumu. Ukomo wa uwakilishi wa viti maalumu, kama ungekuwa vipindi viwili tu, ungewezesha
wanawake wengi kwenda kushindana majimboni/katani, na kutoa fursa ya kada
nyingine ya wanawake kupata uzoefu wa kisiasa. Mpangilio huu ungesaidia kupiga
hatua za msingi na za haraka katika kufikia 50/50.
Kuna hoja kuwa wabunge ni wabunge na madiwani ni madiwani, hivyo
kama mbunge wa jimbo/diwani wa kata hana ukomo pia mbunge/diwani wa viti maalum
asiwe na ukomo ikiwa tu ataendelea kushinda kura za wale wanaowapigia kura. Tukumbuke
kuwa wanawake viti maalumu japokuwa wana majukumu ya kibunge/kidiwani pia wanatumikia
lengo la nyongeza. Wako katika viti hivyo ili kupata uzoefu utakaowawezesha kushiriki
katika siasa za ushindani, kwa hiyo wanawake wengi zaidi inabidi wapate fursa
ya kupata uzoefu huo. Kuwekwa kwa ukomo wa kuwa mbunge wa kiti maalum kutaendana
na malengo ya kuanzishwa vitu maalum katika kifungu namba 4 cha CEDAW kinachotambua
juhudi hizi kuwa ni hatua za mpito ili kurekebisha changamoto ambazo zimekuwa
zikiwakwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika vyombo mbalimbali vya
maamuzi. Kutokuwa na ukomo wa kisheria ama kikanuni kunawapa wanawake walio katika
viti maalumu faida ya ziada katika kuendelea kuhodhi viti hivyo, kwa kuwa wana
mtandao mkubwa katika chama na katika mabaraza ya wanawake ya vyama, faida ambayo
wanawake wanaowania viti maalumu kwa mara ya kwanza hawana. Hili suala la
uhodhi wa viti maalumu ni la vyama vyote, lakini kwa kutumia nafasi yake kama
chama tawala CCM inawajibu wa kutenda kwa mfano, ili kuhakikisha viti maalumu
vinatekelezwa kwa namna inayokidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake hususani
kuwapa wanawake wengi fursa ya kupata uzoefu wa kisiasa kuelekea majimboni.
Maboresho Viti Maalumu
Kutokana
na changamoto tajwa hapo juu, njia ya kwanza ya CCM kutekeleza ahadi yake
katika kifungu cha 168(a) cha Ilani ya Mwaka 2015-2020 ni kuielekeza serikali
hususani Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Ttawala Bora na Haki za Binadamu
ili vijadiliane na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ambayo kikatiba inamamlaka ya
kupokea orodha ya wanawake wanaopendekezwa na vyama vya siasa kushika nafasi za
viti maalumu kulingana na uwiano wa kura wanazo pata, kuwa ili kuendana na
malengo ya uanzishwaji wa viti maalum, majina yanayopendekezwa kwenye Tume ya
Uchaguzi yasiwe ya wale wanawake waliokwisha kuwa kwenye viti maalumu kwa Zaidi
ya vipindi miwili. CCM kama chama tawala
kiwe mfano wa kuwapa kipaumbele na kuweka ulazima wa wanawake waliokaa viti
maalumu kwa zaidi ya vipindi viwili ili wagombee majimboni. Nafahamu kuwa
mabadiliko haya yatapata pingamizi kubwa, hasa kutoka kwa wanawake wenyewe,
lakini ukweli utabaki kuwa ukweli. Hivyo basi, kama njia ya kuwapa motisha
wanawake waliokaa kwenye viti maalumu zaidi ya vipindi viwili, kuwekwe hatua
ya mpito, kwa wanawake hawa kuhakikishiwa kuwa ikitokea wameshindwa
uchaguzi, basi watapewa kipaumbele katika nafasi za viti maalum zitakazopatikana
kwa CCM. CCM ina fursa ya kuweka ukomo
wa viti maalumu katika kanuni za uchaguzi ambazo naamini zitafanyiwa
marekebisho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020.
Napendekeza pia CCM ielekeze vyombo husika kufanya utafiti na
majadiliano na vyama vya siasa ili kuweka Kanuni zitakazo tumika na vyama vyote
katika kuwapata wanawake viti maalumu kwa kuwa kwa sasa kila chama kina
utaratibu wake, suala linaloibua maswali juu ya upatikanaji wao. Japo inafahamika
kuwa sifa ya mbunge ni kujua kusoma na kuandika, kwa upande wa viti maalumu hatua
kwa hatua ya namna wanawake hawa wanavyopatikana ni muhimu katika kuwapa imani
wananchi juu ya matumizi ya kodi zao kwa ongezeko la idadi ya wabunge wa viti
maalumu. Pia kuhakikisha wanawake wanaochaguliwa wana sifa na uwezo wa kusaidia
kufikia malengo ya kuanzishwa kwa viti hivyo.
Japokuwa maboresho hapo juu, yatavifanya viti maalum kuwa na tija
na hivyo kufikia malengo ya kuanzishwa kwake. Kusipokuwa na juhudi za ziada,
itachukua muda sana kufikia 50/50. Kama baada ya miaka 34 ya kuanzishwa kwa
viti maalumu ni wanawake asilimia 7 tu ndio wameweza kushinda majimbo ya
ubunge, hesabu ya haraka inaonyesha unahitaji miaka mingine 102 ili kuweza
kufika idadi ya asilimia 50 ya wanawake bungeni, na hii ni katika mpangilio wa
asilimia 30 viti maalumu na asilimia 20 kutoka majimboni. Hivyo kama CCM haitachukua
hatua za ziada utekelezaji wa kifungu 168(a) kuhusu 50/50 ifikapo 2020 ni ndoto.
Hivyo, sambamba na uboreshaji wa viti maalum, njia nyingine ya kuongeza idadi
ya wanawake ni kupitia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambapo kwa kutumia
sheria mpya ya vyama vya siasa, ambayo inaweka sharti la vyama vya siasa
kuanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia pamoja na mambo mengine, usawa wa
kijinsia, CCM inaweza kuishauri serikali imshauri Msajili wa Vyama vya siasa
kuweka katika kanuni za sheria ya Vyama vya Siasa zinazo endelea kutungwa, kifungu
kinacho hakikisha kuwa asilimia fulani ya wagombea ni wanawake, sana sana
asilimia ishirini, ili kujazia nafasi inayo achwa na viti maalum. Itakuwa jambo
la msingi, NEC wangetenga majimbo asilimia ishirini ambayo watagombea wanawake pekee.
Hivyo kutakuwa na asilimia 30 ya viti maalum, asilimia 20 ya majimbo ambayo
watagombea wanawake hivyo kutimiza 50/50. Mfumo wa kutumia viti maalumu
sambamba na majimbo ya wanawake pekee inatumika katika nchi jirani kama Rwanda na
Kenya.
Mbadala wa Viti Maalum
Japo
viti maalumu vinaweza kuboreshwa kama ilivyopendekezwa hapo juu na kutuletea
50/50, kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala kama bado tuna hitaji viti maalumu,
au kama nchi tunaweza kuwa na mfumo bora wa kuwezesha wanaume na wanawake
kushiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi. Nakumbuka imeshasemwa kuwa suala
la katiba mpya, japo muhimu, lakini siyo kipaumbele kwa wakati huu. Hivyo mapendekezo
hapa chini yanajikita kwenye uelewa kuwa yanaweza kuwekwa katika Katiba ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama mabadiliko madogo (miscellenious
amendment) ili kuweka utaratibu utakaosaidia kuifikia 50/50. Nikiongozwa na
usemi wa ‘Msema kweli ni mpenzi wa Mungu.’
Napendekeza kuwa viti maalumu vinahitaji mbadala haraka iwezekanavyo. Asimia 30
ya wanawake bungeni sio lazima iwe viti maalumu, inaweza ikatafsiriwa katika
majimbo na kata, yaani asimilia 30 ya majimbo na kata zote za uchaguzi wagombea
wawe ni wanawake peke yao, kila chama kisimamishe mwanamke kama mgombea katika
majimbo na kata hizo. Na wale wanawake wenye uwezo wa kugombea katika majimbo
yasiyo ya wanawake waruhusiwe kufanya hivyo. Japo pendekezo tajwa hapo juu ni
zuri, lakini halitatufikisha kwenye 50/50 inayo ahidiwa na kifungu cha 168(a)
cha Ilani ya CCM 2015-2010. Hii inanilazimu nitoe hoja mbili kama mbadala wa
viti maalumu; -
Mosi, ni kugawanya idadi ya majimbo na kata zilizopo mara mbili
(ili kutoongeza ukubwa wa bunge/baraza la madiwani). Katika kila jimbo na kata kila
chama kinasimamisha mgombea mwanamke na mwanaume. Mpiga kura anapokuwa
amechagua chama fulani anakuwa amechagua mgombea mwanamke na mwanaume kutoka
chama hicho. Hivyo baada ya uchaguzi unapata uwakilishi wa 50/50 kwa wanawake
na wanaume katika kata na majimbo. Mbadala wa pili, ni kubadili mfumo mzima wa
uchaguzi kutoka utaratibu wa jimbo au kata moja kuwa na mwakilishi mmoja yaani First Past the Post (FPTP) mpaka
uwakilishi wenye uwiano sawa yaani Proportional
Representation (PR). Mfumo huu unatakiwa uende sambamba na sharti la kutaka
orodha ya wawakilishi wa vyama katika majimbo na kata kuwa na idadi sawa ya
wanawake kwa wanaume kwa kufuata mfumo wa pundamilia yaani Zebra System. Faida zinazoendana na kuweka mbadala wa viti maalumu,
ni pamoja ya kuiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi. Hii ni kwa sababu
wanawake watakuwa wakitokea katika asilimia kadhaa ya majimbo na kata halisi,
na si kama nyongeza juu ya namba halisi ya madiwani au wabunge. Serikali
itaokoa Trilioni za shilingi ambazo zinazitumia sasa katika kulipa mishahara,
posho na vi-inua mgongo kwa wanawake viti maalumu wakiwa kama nyongeza ya
wabunge na madiwani halisi. Pia mbadala huu utaondoa maswali kutoka kwa wana
jamii ya je wanawake viti maalumu wanamwakilisha nani, kwa kuwa sasa watakuwa
wanatokea kwenye majimbo na kata. Watapata haki ya moja kwa moja ya kupata fedha
za maendeleo ya jimbo na wataweza hata kuwa waziri mkuu kwa kuwa wana vigezo. Changamoto
za madiwani viti maalumu kutoruhusiwa kuwa wenyeviti/mameya wa halmashauri na
kamati za kata, na masharti ya kutokuwa wajumbe katika kamati za maadili, fedha,
na kukaimu uwenyekiti wa kamati za maendeleo ya kata zitaondoka.
Hitimisho
Katika
harakati zangu na kuonana na kuchota maarifa na maono ya watu mbalimbali juu ya
suala hili, kuna mtu alinambia kuwa ‘Chama
kina vipaumbele vingi, kama suala halina madhara kwa chama, nguvu na msukumo wa
kufanyia kazi suala hio inakuwa haipo.’ Najitolea kupuuza ushauri wake kwa
kuwa naamini suala hili nyeti na lenye tija kwa wanawake, ambao ni walezi wa
taifa hili, wapiga kura wengi na waaminifu. Nina Imani CCM chini ya uongozi wa
Mwenyekiti na Katibu Mkuu wake itafanyia kazi mapendekezo haya. Muda umefika
tufunge huu mjadala ili wote wanawake na wanaume tubaki kuchapa kazi.
Wasalaam- Victoria Lihiru- Mwanafunzi shahada ya Uzamivu Chuo Kikuu Cape Town, Afrika Kusini. Napatikana kupitia victorialihiru@gmail.com, +255 713 085 139
No comments:
Post a Comment