Nicodemus Minde-@decolanga
Ni karibu wiki moja tangia Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti Jaji Mstaafu Joseph Warioba kuzindua rasmi rasimu ya Katiba. Mijadala miongoni mwa Watanzania wengi imekua ni mfumo wa serikali, mazungumzo ya muungano, madaraka ya rais, umri wa rais, na mengine mengi. Nimefuatilia mazungumzo mengi yaliyotokana na uzinduzi huu wa rasimu ya katiba. Ninafuraha kubwa kuona muamko mpya wa majadiliano miongoni mwa Watanzania kuhusianana na rasimu hii. Hakika, Tanzania ipo katika mpito wa mafanikio. Tunamshukuru Mungu.
Wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikipokea maoni, moja kati la swala kuu lililovuta hisia ya Watanzania wengi ni lile la lugha ya taifa, Kiswahili. Hata kabla ya mchakato huu wa katiba, kulikua na mijadala kuhusiana na sehemu ya lugha ya Kiswahili kwenye elimu ya Tanzania, na katika Katiba Mpya kwa ujumla. Sekta mbali mbali pamoja na asasi mbali mbali za kieleimu zilitoa mapendekezo yao. Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) walisisitiza umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwenye elimu. Hivi karibuni, nchi ilishtushwa na matokeo duni ya Kidato cha Nne (Soma ufafanuzi hapa). Wananchi walizungumza kwa kina kuhusu sababu za kufeli kwa wanafuzi, asasi mbali mbali pamoja na idara za serikali walitoa sababu zao. Hivi karibuni, Twaweza, ambalo ni shirika la kiraia lilitoa tathmini kuhusiana na kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne. Moja ya jambo lililopewa kipaumbele ni matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye ngazi ya sekondari.
Kwenye ibara ya nne ya rasimu ya Katiba, lugha ya Kiswahili inapewa kipaumbele cha juu. Kifungu cha kwanza katiba ibara hii inaeleza kwamba: Lugha ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano ni Kiswahili na itatumika katika mawasiliano rasmi ya kitaifa na kiserikali. Kifungu cha pili kinaeleza: Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ndogo ya (1), lugha ya Kiingereza inaweza kutumika kuwa lugha rasmi ya mawasiliano ya kiserikali pale itakapohitajika.
Kwa mtazamo wangu, maelezo na mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Warioba kuhusiana na Kiswahili ni bora. Kwanza, utambulisho wa Mtanzania ni ule unaotokana na ufasiri wa lugha, uongeaji wa lugha ya Kiswahili na juu ya yote utofauti wetu unaotokana na uongeaji wa Kiswahili. Wale wanaopinga matumizi ya Kiswahili sababu yao kuu ni sehemu ya Tanzania miongoni mwa mataifa ya dunia. Wanasema Watanzania watabaki kuwa waongeaji wa Kiswahili wakati lugha ya biashara, lugha ya uhusiano wa kimataifa ni Kiingereza. Rasimu ya Katiba imeweka wazi kwamba lugha ya Kiingereza inaweza tumika katika mazingira ya kipekee.
Swali kuntu hapa ni je, Kiswahili kibaki kama lugha rasmi, ya kiofisi na lugha ya kufundishia? Ama tubadilishe na tutumie Kiingereza kama lugha ya kufundishia? Ama zote zitumike kwa mkupuo? Hakika kazi tunayo ili kupata muafaka.
No comments:
Post a Comment