Ngasa dhidi ya Manchester United |
Nicodemus Minde
Kocha wa zamani wa Brazil Dunga aliwahi kumfananisha Mrisho Ngasa na Robinho. Ngasa ni moja kati ya wachezaji bora Tanzania imewahi kujivunia kwa miaka ya hivi karibuni. Ngasa anapiga chenga, anakasi hatari, anaujuzi wa mpira, anafurahisha jukwaa kwa chenga za maudhi. Licha ya ufupi na umbo dogo, Ngasa anauwezo mkubwa. Sikushangaa Dunga akimsifia. Makocha wengi wamemsifia. Ni wazi vilabu vikubwa vya Brazil vilikua vilimtaka winga huyu hatari baada ya kumsumbua beki nguli Lucio, Brazil ilivyocheza na Tanzania kabla ya michuano ya Kombe la Dunia 2010. Giofranco Zola naye alimuita Ngasa afanye majaribio Westham. Seattle Sounders ya Marekani nayo ilimuita afanye majaribio. Nakumbuka vizuri tarehe 20 Julai 2011 mechi kati ya Seattle Sounders dhidi ya Manchester United. Ngasa aliingia kwenye dakika kumi na tano za mwisho. Aliisumbua Manchester na hususan Rafael. Jamaa alipongezwa sana. Kwenye mashindano ya Challenge jijini Nairobi, Ngasa aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo. Ngasa alikua mhimili mkubwa wa timu ya taifa katika mashindano mengi.
Kwa sifa hizi kedekede, Mrisho Ngasa alinyakuliwa na matajiri wa Azam FC. Sawa, nilielewa ni ajira na maslahi yaliyompeleka Ngasa Azam akitokea Yanga. Alicheza vizuri na timu yake ya Azam licha ya kelele za hapa na pale eti yeye bado ni Yanga damu. Juzi hapa, timu yake ya Azam ilifika kwenye fainali ya michuano ya CECAFA ya Kombe la Kagame. Ngasa amekua akitumiwa sana kama mchezaji wa akiba na kocha Stewart Hall. Naskia jambo hilo halijamfurahisha Ngasa. Yanga iliifunga Azam 2-0 kwenye fainali hiyo. Picha za Ngasa akiibusu beji ya Yanga zilitapakaa kwenye mitandao na magazeti. Azam, kwenye ukurasa wao wa Facebook walitangaza kutoa nafasi ya upendeleo kwa Yanga kwa madai kuonyesha nia ya kurudi klabu yake ya zamani. Magazeti ya Tanzania yanaripoti kwamba Simba pia wanamtaka Ngasa.
Ngasa akibusu jezi ya Yanga |
Katika upekuzi wangu wa magazeti ya Uingereza, nimevutiwa na habari ya Victor Mugubi Wanyama, kiongo wa Celtic ya Scotland kuhitajiwa na vilabu vikubwa vya Uingereza. Manchester United na City zinamtaka huyu kijana ambaye ni mdogo wake kiungo wa zamani wa Inter Milan MacDonald Mariga. Arsenal pia wanamuangalia huyu yosso. Nilikaa nikajiuliza hivi huyu Wanyama ananini ambacho Ngasa hana, labda umbo kubwa tu. Labda ana bahati tu!. La hasha, huyu kijana anajituma. Anajua kiwango chake ni cha Ulaya. Mpira wake sasa ni wa ligi kubwa kama za Uingereza, la Liga, n.k. Sijui Ngasa anajua hili?
Kama tunavyosema Tanzania: Yangu macho tu! Simba wamehaidi kutoa Tshs. 25m, Yanga wanataka kutoa Tshs.20m. Celtic wanasema Wanyama anathamani ya pauni 7m. Kwa hela zetu hapa ni Tshs. 17.5b. Sawa bwana.
No comments:
Post a Comment