Monday 7 April 2014

Ujana, Usasa, Udijitali; Namkumbuka Monika wa Mwisho wa Kosa!

Jana, Jumapili, jua angavu na hali ya hewa tulivu. Nipo katika shughuli zangu za kawaida za Jumapili. Natizama mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza, Everton wanacheza na Arsenal huku nikifuatilia kwa utaratibu mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye simu yangu ya kiganjani kupitia mitandao ya kijamii. Yanga inacheza na JKT Ruvu huku timu ya vijana ya Tanzania - Ngorongoro Heroes wanakipiga na Kenya. Mara napata simu. Ni mzee wangu anauliza niko wapi. "Nipo hapa Sakina natizama mechi baba," namjibu huku Everton wanapiga goli la tatu. Dah! Vipi tena Arsenal? Mporomoko huu sio mchezo. Rafiki yangu pembeni ananiambia nisishangae ni kwmba wanarudi ile nafasi yao wanayoipenda - nambari nne! Shabash! 

Baba anataka twende naye kumwona ndugu yetu mgonjwa. Nasita kidogo kwani Liverpool ndio wanaingia uwanjani Upton Park kucheza na Westham. Kaida yangu nikutizama mechi zote. "Sawa baba, we nikute hapa twende kumwona mgonjwa" namjibu kwa shingo upande. Baada ya dakika 15 hivi bado milango migumu kwa timu zote, natoka baada ya baba kufika pale Sakina. Napanda gari, mama naye yuko. Namsalimia na tunaondoka kwenda kumwona mgonjwa nyumbani kwake. 

Ndugu wengine wamefika nyumbani kwa mgonjwa kumpa pole baada ya kulazwa kutokana na presha kupanda ghafla. Tunasalimiana kwa bashasha, furaha kama kawaida ya Watanzania. Baada ya kumpa pole mgonjwa hadithi zinanoga. 

"Mara ya mwisho kukoona ulikuwa mdogo sana vipi habari yako?" wananiuliza. Natabasamu tu. Katika maongezi yetu pale suala la ndugu kutotembeleana linaibuka. Ujana, usasa na udijitali unatajwa kama sababu ya mkengeuko huu. Nakumbuka kwa haraka riwaya ya Mwisho wa Kosa iliyoandikwa na Z. Burhani. Tuliisoma riwaya hii na kutahiniwa Kidato cha Nne. Namkumbuka mwalimu wetu Bwana Mugambi na Mama Shihemi, walikuwa bora sana. Monika, mhusika mkuu alitoka Ulaya masomoni na kurudi nyumbani na usasa, ujana na ujiditali kama inavyofahamika nyakati hizi. Monika alijishaua, alijibetua na kujidahi kuwa hawezi hata kunywa uji wa Bi. Keti. Yote ni kutokana na usomi na elimu ya magharibi. Maongezi yetu ya jana yalinikumbusha Riwaya ya Mwisho wa Kosa na mkasa wa Monika huku nikijilinganisha.

Hakika kizazi cha siku hizi, sio tu cha vijana bali hata wazee wa kisasa. Tumesahau tulikotoka huku tukikumbatia usasa. Tumesahau utamaduni wetu, watu wanakutana kwenye mazishi tu. Ndugu wamesahauliana kabisa. "Yaani niko busy sana!" ndio kauli zetu. Lakini kama Z. Burhani anavyosema Mwisho wa Kosa ni pale Monika aligundua usasa na ujana ni mpito; utamaudini wake unabaki pale pale. Tuenzi utamaduni wetu, lugha yetu na falsafa ya Kiafrika! Majuto mjukuu huja baadae!

2 comments:

  1. hehe interesting.
    i hate it when you people they say they are busy. They are trying to imply that they have no time even to visit their relatives or to stay with their families. I believe its lack of balance. We embrace modernity and we become so absorbed into its wonders that we have almost as if forgotten what it means to be a social being.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Thank you so much for the comment. As you rightly put it, we have embraced modernity at the expense of our traditional values! Thank you once again for the comment!

      Delete

[ZELEZA] Malawi’s Political Earthquake: Nullification of the Presidential Elections

By Prof Paul Tiyambe Zeleza  3/2/2020 The Malawian Constitutional Court has annulled last year's presidential election results....

Most Viewed